Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Jamaa wawili waliopatikana na pembe moja za ndovu yenye thamani ya shilingi milioni tatu walisomewa mashataka baada ya uchunguzi dhidi yao uliochukua takribani siku kumi kukamilika.

Ali Omari Hajj na Said Alfani Mwinyi waliyakanusha mashtaka ya kupatikana wakiuza pembe hizo katika eneo la Mama Ngina mjini Mombasa mnamo tarehe 27 mwezi Disemba mwaka jana.

Ombi lao la kutaka kuachiliwa kwa dhamana lilipingwa na kiongozi wa mashtaka Lydia Kangori, huku akisema kuwa atawasilisha cheti maalum kinachoorodhesha sababu za kupinga dhamana hiyo hapo kesho.

Kesi hii itarudi tena mahakamani siku ya Alhamisi ili kuamuliwa iwapo wawili hao wataweza kuachiliwa kwa dhamana au la.

Wakati huo huo, jamaa mmoja aliyepatikana na magamba ya risasi 507 pamoja na bunduki bila leseni ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki moja au pesa taslimu shilingi elfu hamsini na hakimu mkuu Diana Mochache.

Noor Mohammed amekanusha mashtaka kuwa mnamo tarehe 5 mwezi huu katika eneo la Buxton mjini Mombasa alipatakana na vifaa hivyo vinavyoaminika kutumika katika utovu wa usalama.

Kesi hii itaskizwa tarehe 23 mwezi Machi mwaka huu.