Washukiwa wanne wa ujambazi walitiwa mbaroni katika eneo la Old Town jijini Mombasa, Jumatatu.
Maafisa wa serikali ya Kaunti ya Mombasa waliwatia mbaroni washukiwa hao waliokisiwa kuwahangaisha wakaazi katika mitaa ya Old Town.
Kulingana na mkuu wa usalama katika Kaunti ndogo ya Mvita, Waziri Sudi, vijana hao walishikw usiku wa kuamkia Jumatatu.
“Hawa vijana wamekuwa wakiwahangaisha wananchi wa eneo hilo hasa nyakati za usiku”, alisema Sudi.
Aliongezea kuwa wanne hao walikuwa miongoni mwa genge la vijana 35 wenye umri kati ya miaka 16 na 25.
Sudi alisema walinaswa wakiwa na kilo mbili za bangi pamoja na visu, mapanga na bunduki bandia wanazotumia kuibia watu kwenye mitaa ya Kibokoni na Kuze.