Jamii ya Wamaasai ambao hawana mahali maalum pa makazi katika kaunti ya Mombasa wameitaka serikali kuu na ile ya kaunti kuwahakikishia usalama wao na mifugo wao huku tayari kukianza kushuhudiwa kunyesha kwa mvua ya El Nino.
Wamesema kuwa mifugo yao iliweza kuangamia katika mvua ya masika iliyonyesha kwa miezi miwili mwaka wa 2012 ambapo walipata hasara kubwa na hakuna fidia waliwahi kupewa na serikali ya taifa na wakasisitiza kuwa hawapo tayari kuona hasara nyingine sawa na hiyo.
Wazee pamoja na vijana wa Moran hao wakiongozwa na Mzee Loilel Sankara siku ya Jumapili kwenye eneo la Vijiweni Mombasa, ambako wameweka makao ya muda, walisema kuwa tayari wameanza kupoteza baadhi ya mufugo wao kama vile ndama wanaozaliwa kwa sababu ya kunyeshewa na kupata maradhi ya kichomi pia kondoo wao pamoja na mbuzi.
Bw Loileli alitoa hofu kuwa huenda wakapata hasara kubwa iwapo yale waliosikia kutoka kwenye idara ya hali ya anga kuhusiana na mvua ya El Nino ni kweli.
Alisihi hasa serikalu ya kaunti kupitia idara inayosimamia masuala ya dharura na majanga, kuangazia wito wao na kuwapa nafuu, ndipo na wao wajione kama jamii nyingine humu nchini.
"Sisi jamii ya Maasai tumetengwa na serikali kwa muda mrefu, naomba rais wetu Uhuru Kenyatta na msaidizi wake kutukumbuka na tupewe mahali pa kukinga hawa mifugo wetu wasiuliwe na maji ya mvua pamoja na maradhi yatakayosababishwa na baridi," alisema mzee Loilel.
Kwa mwelekeo mmoja, walisihi serikali kununua mifugo wao iwapo mvua hiyo itakuwa nyingi ili kuwaepusha na kupata hasara kwa kufa kwa mifugo badala yake serikali iwanunue kupitia idara ya nyama KMC.