Jamii ya Mijikenda wanaomiliki mashamba eneo la Pwani wamehimizwa kutokubali kulaghaiwa na baadhi ya mabwenyenye na kuuza mashamba yao kiholela.
Jamii hiyo imetakiwa kutunza raslimali hizo ili ziwasaidie katika siku za usoni.
Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amesema kuwa ni wakati wa jamii hiyo kuwa waangalifu na watu kama hao ili kuhakikisha kuwa mashamba hayo yanasaidia vizazi vijavyo katika jamii hiyo.
Akizungumza katika mtaa wa Maweno, eneo bunge la Nyali siku ya Jumatano, Awiti alisema kuwa kuendelea kushuhudiwa kwa mizozo ya ardhi katika eneo la Pwani kumechangiwa na baadhi ya wazee wa jamii hiyo kuuza mashamba yao kiholela kutokana na kukithiri kwa umaskini.
Mbunge huyo ameishinikiza Tume ya Ardhi nchini (NLC) kuhakikisha kuwa inatatua swala la mizozo ya ardhi na kutoa hati miliki za ardhi kwa jamii hiyo ili kuzuia unyakuzi wa ardhi unaotekelezwa na baadhi ya mabwenyenye katika eneo la Pwani.
"Tunaitaka Tume ya Ardhi nchini NLC kuhakikisha kuwa swala la mizozo ya ardhi katika eneo la Pwani linasitishwa. Wazee wa jamii ya Mijikenda mskikubali kudanganywa kuuza ardhi zenu. Tafadhali ziwekeni kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Awiti.