Viongozi wa jamii ya Ogiek wilayani Njoro na Kuresoi Kusini wanaitaka serikali kuzingatia usawa wa kimaeneo katika uteuzi wa watumishi wa umma ili kudumisha umoja wa kitaifa. Wito huu umetolewa na aliyekuwa diwani wa Tinet, David Sitienei, ambaye ameteta kwamba jamii zenye idadi ndogo ya watu hazina usemi katika serikali ya muungano wa Jubilee haswa katika utoaji wa nafasi za kazi. Aliteta kuwa Ogiek ni miongoni mwa jamii ambazo husahaulika sana panapo zoezi la kuwaajiri watumishi wa umma licha ya kuwa na wenyeji waliofaulu katika elimu ya juu na kutimiza kanuni na masharti yote yanayohitajika ili kuajiliwa. Akiongea na waandishi wa habari mjini Molo, Sitienei alisema kuwa baadhi ya vipengele kwenye katiba vimepuuzwa kwani hata vyama vya kisiasa vilikosa kutimiza sheria ya kuwapa watu wenye mahitaji maalum na jamii zilizotengwa, nafasi katika uongozi kupitia uteuzi. Kiongozi huyo amesema katika takwimu za wafanyikazi wa serikali ikiwemo waalimu, madaktari, idara ya usalama miongoni mwa kazi zingine, jamii ndogo hukosa waakilishi wanao hitimu kwa sababu ya kisiasa na kikabila. Amesema kuwa viongozi wenye umaarufu hutetea wananchi wa makabila yao ili wapate kazi huku viongozi wengine pamoja na wasimamizi wa uteuzi wakidai hongo ili kupeana nafasi za kazi. Sitienei alisema swala la utoaji ajira linafaa kusawazishwa ili kuhakikisha kila jamii inahisi kushirikishwa katika vitengo vyote vya uongozi kwenye serikali kuu na zile za majimbo.

Share news tips with us here at Hivisasa