Jamii ya walemavu katika kaunti ya Mombasa imeombwa kujitokeza na kujitosa katika ulingo wa kisiasa ili kuwasiadia wenzao hasa katika maswala ya uwakilishaji katika ngazi za kitaifa.
Afisa wa haki na sheria katika shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini la Haki Afrika, Francis Auma Gamba alisema kuwa wakati umefika sasa kwa jamii hiyo kuonyesha ukakamavu wao na kujiunga na mchakato wa kisiasa ili kubadilisha maisha ya jamii hiyo kutokana na kuwa wengi wao wanadai kukandamizwa na kutengwa na baadhi ya viongozi hata baada ya kuwachagua.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano katika mkuatano wa Jamii hiyo ya Walemavu, Auma alisema kuwa iwapo walemavu watajitokeza waziwazi na kupigania nyadhfa mbalimbali za kisiasa basi jamii hiyo itakuwa na viongozi watakaowawakisha vyema serikalini.
"Tafadhalini ndugu zangu wakati umefika sasa wa nyinyi kujitokeza kwa wingi na kuungana na kumchagua kiongozi atakayewawakilisha vyema serikalini na katika bunge la kitaifa ili maswala yenu muhimu yawezekuwakilishwa bila vizuizi vyovyote," alisema Auma.
Mapendekezo ya mwahanarakati huyo ilijiri baada ya jamii hiyo kulalamikia kukandamizwa na baadhi ya viongozi nchini sawa na serikali kuu na zile za kaunti na kukosa kusaidika vyema.