Jamii ya wamaasai sasa imeapa kupinga ujenzi wa reli mpya ya kisasa SGR itakayopitia katika ardhi yenye utata ya Kedong mjini Naivasha kaunti ya Nakuru.
Aidha jamii hiyo imeonya pia itasimamisha ujenzi wa eneo la kuegesha magari pamoja na miradi ya mvuke inayofanywa kwenye ardhi hiyo yenye ukubwa wa ekari 77,000.
Hayo yaliibuka wakati wa maandamano yaliyofanywa Ijumaa na zaidi ya watu 500 wa jamii hiyo huku wakiifunga barabara ya Mai Mahiu kuelekea Narok eneo la Suswa.
MCA wa eneo hilo Kipas Lengues amesema kuwa swala la ardhi hiyo liko mahakamani, na kushangaa ni kwa nini usimamizi wa Kedong umeweka ilani kwenye magazeti ya humu nchini.
“Tunawataka wafadhili wa mradi huu wa SGR kukoma kuufadhili tena hadi pale swala la umiliki wa ardhi hiyo litakapotatuliwa” akasema mkaazi Mike Ole Roka.
“Tumeishi eneo hili tangia kuzaliwa kwetu, na sasa nina watoto watano wote wakubwa; tunatakiwa kuondoka hapa twende wapi?” akahoji bii Lillian Leson.