Jamii ya Wanubi humu nchini inakabiliwa na matatizo ya ardhi licha ya jamii hiyo kujitahidi katika kupigania raslimali zao hususan ardhi kwa muda mrefu bila ya mafanikio.

Share news tips with us here at Hivisasa

Msimamizi wa maswala ya kijamii katika jamii hiyo nchini Khadijah Ali Asman amesema kuwa tatizo hilo la ardhi limepelekea Wanubi wengi kushindwa na kumiliki angalau kipande kidogo cha ardhi.

Akiyafichua hayo katika bustani ya Mama Ngina mjini Mombasa siku ya Jumapili, wakati wa tamasha la kitamaduni la kabila hilo, Khadija amesema kuwa kabila hilo halitasita kupigania haki zao za ardhi kutoka kwa serikali na kuishinikiza kuikabidhi ardhi jamii.

“Sisi kama jamii ya Wanubi tunapitia changamoto nyingi hususan ukosefu wa ardhi na tumepigania swala hilo kwa muda mrefu bila ya mafanikio yoyote licha ya serikali kulitambua hilo lakini la kustajabisha ni kuwa hatujaona kama serikali inatutambua kama makabila menyinge nchini, ndiposa tunataka serikali itutengea na sisi ardhi,” alisema Khadija.

Khadija ameitaka serikali kuwahusisha Wanubi katika maamuzi yote muhimu yanayohusiana na uongozi na maendeleo ya nchi na wala sio kulibagua kutokana na uchache wa watu wa kabila hilo.

Shamra shamra hizo za jamii ya Wanubi zitaendeleza katika bustani ya Mama Ngina hadi siku ya Jumapili ambapo utamaduni wa kabila hilo ukiwemo maonyesho ya vyakula, mavazi, urembo utakapofika tamati.