Kituo cha kuwarekebisha tabia watumizi wa mihadarati cha ‘Reach out centre trust’ kimaitaka jamii ya Mombasa kuhudhuria vituo vya kupima virusi VCT kwa hiari ili kujua hali zao za kiafya.
Akizungumza katika kituo hicho mjini Mombasa siku ya Jumatatu, afisa wa maswala ya kupima virusi katika Shirika hilo Sheillah Abdillahi Issah amesema kwamba Vijana wengi wamehofia kuzuru vituo hivyo licha ya hali ya maambukizi ya virusi kuongezeka katika Kaunti ya Mombasa.
Akikiri kwamba sio rahisi kwa vijana kuhudhuria vituo hivyo vya kupima virusi kwa hiari, Abdilahi amesema kwamba Shirika hilo limewekeza mbinu mwafaka zinazowafaa vijana ili wakubali kupimwa virusi kwa hiari hasa baada ya kubainika kwamba wamo katika hatari ya kuambukizwa virusi vinavyosababisha ukimwi.
Afisa huyo amekiri kwamba ikilinganishwa na watu wazima, Vijana wana mahitaji maalum ili wakubali kwa hiari kupima hali zao za virusi, na akahoji kwamba tayari kituo hicho kinawahudumia Vijana kwa lengo la kumuweka kijana katika mazingira yatakayomuondolea hofu ya kupima virusi kwa hiari.
"Tunawaomba vijana na jamii kwa jumla kujitokeza na kutembelea vituo vya kurekebisha VCT kupima virusi kwa hiari ili kujua hali yao na jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi," alisema afisa huyo.
Hata hivyo, Afisa huyo wa kupambana na maambukizi ya ukimwi amekiri kwamba katika siku za hivi majuzi, wakazi wa kaunti hiyo wamekuwa wakijitokeza ili kujua hali zao za virusi hasa ikizingatiwa kwamba watu wawili hufariki kila siku huku wengine watatu wakiambukizwa virusi kila uchao katika Kaunti ya Mombasa kulingana na takwimu za baraza la kupambana na ukimwi nchini NACC.
Picha: Shirika la Kupambana na mihadarati katika ukanda wa pwani, limewataka vijana na jamii kujitokeza katika vituo vya afya kujua hali zao.