Afisa wa mipango katika Shirika la African Institute For Health and Development amesema kuwa mila na desturi mbovu zinafaa kutupiliwa mbali na jamii ili kuhakikisha usawa wa kijinsia hususan kwa wanawake na watoto unatekelezwa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza siku ya Jumamosi na mwandishi huyu mjini Mombasa, Hamisi Dzole, alisema kuwa wanawake pamoja na watoto wamenyimwa haki zao katika familia nyingi.

Dzole alisema kuwa unyanyasaji huo umechangia akina mama na watoto kudhoofika kiafya kutokana na ukosefu wa lishe bora kutoka kwa waume zao.

Afisa huyo alielezea kuwa tayari wana mipango kabambe inayohusisha akina mama, ili kuwapa mafunzo ya kujikimu kimaisha pamoja na kufanya ukulima ili kupata lishe bora na kuhakikisha afya ya watoto wao imeboreshwa.

“Tumepanga mikakati maalum ya kuhakikisha kuwa jamii inapata lishe bora kwani tumebaini kuwa wanaume wengi wameacha familia zao zikiteseka kwa kuwanyima chakula na kuwanyima huduma za afya,” alisema Dzole.

Dzole aidha alisema kuwa mradi huo wa 'Empowerment Of Nutrition Improvement For Women and Children' ulioanzishwa mwaka wa 2013 katika eneo la Chaani kwa ushirikiano na serikali, utawasaidia kutatua changamoto hizo.