Wito umetolewa kwa jamii kuukumbatia mpango wa elimu ya Teknolojia kama njia mojawapo ya kuinua ubunifu na kuimarisha uchumi wa taifa hili kupitia sekta mbalimbali.
Katika mahojiano ya kipekee afisini mwake Jumatatu, Mkurugenzi wa chuo kikuu cha Mount Kenya Tawi la Nakuru Dkt Pamela Ochieng' alisema kuwa mpango huo ni muhimu katika ufanisi wa taifa hasa ikizingatiwa mhemko mpya wa maswala ya maendeleo ya Teknolojia.
Isitoshe, alikiri kwamba wameshapokea wanafunzi wengi chuoni humo ambao wamejisajili kwa mpango huo kupitia Bodi ya Mpango huo KICTP chini ya uwenyekiti wa Dkt Samuel Wambugu.
"Katika Chuo hiki tawi la Nakuru tumepokea wananfunzi zaidi ya 1,000 ambao wamejisajili kupitia mpango huo, na letu ni jukumu la kuhakikisha wanapata elimu bora katika maswala ya teknolijia ICT''alisema Ochieng'.
Aliongeza kuwa mpango huo ukitumiwa vyema utasaidia katika kuzalisha nafasi za ajira hata miongoni mwa vijana ambao baada ya maarifa ya Teknoljia watakuwa wabunifu katika sekta mbalimbali.
Na huku hayo yakijiri, vijana zaidi ya 2,000 wamefaidika na mpango huo wa ICT kutoka eneo bunge la Nakuru mjini Mashariki chini ya ufadhili wake Mbunge David Gikaria kwa ushirikiano na KICTP.
Katika mahojiano na mwenyekiti wa mpango huo katika afisi ya Mbunge huyo Bwana Naftali Nyambegera, wanaosajiliwa huitajika tu kulipa shilingi mia nane ya mtihani na kisha kupata elimu hitajika.
"Mpango huu umeshang'oa nanga na langu ni kuwarai tu wakazi vijana, wazee na akina mama kuhakikisha kwamba wanatumia fursa hii kupata elimu ya teknolijia ambayo ina manufaa yake katika kipindi hiki," alisema Nyambegera.