Share news tips with us here at Hivisasa

Idadi kubwa ya visa vya uhalifu vinavyotokea katika eneo la Pwani huchangiwa pakubwa na jamii kuficha taarifa muhimu kuhusu wahalifu.

Kauli hii ni kwa mujibu wa naibu kamishna wa Kaunti ya Kwale Moses Ivuto, aliyesema hayo huko Kinango siku ya Jumatatu.

Inadaiwa kuwa mara nyingi wanananchi huwafahamu vyema watu wanaoendeleza uhalifu lakini hunyamaza kimya kutokana na uoga wa kuvamiwa endapo watatoboa siri hiyo.

Afisa huyo wa usalama alisema hali hii imesababisha vifo vingi ambavyo huripotiwa kila mara hasa katika eneo la Kinango, Kaunti ya Kilifi.

“Asilimia 99 ya vifo vinavyoripotiwa katika eneo hili ni kutokana na jamii kunyamazia swala hili, na hii ni changamoto kubwa sana,” alisema afisa huyo.

Wakati huo huo, naibu kamishna huyo aliwasihi wananchi kushirikiana na viongozi wa eneo hilo pamoja na maafisa wa usalama ili kutoa habari zozote kuhusu mtu wanayemshuku huenda analenga kutekeleza uhalifu.

“Tushikane pamoja na viongozi wetu bega kwa bega ili tuone vile tutakomesha uhalifu unaoshuhudiwa hapa,” alisema Ivuto.

Kauli hiyo inakuja huku idara ya usalama katika ukanda wa Pwani ikiwa katika harakati ya kukabili makundi ya vijana yanayodaiwa kuendeleza uhalifu katika maeneo mbalimbali, huku jamii ikiaminika kufahamu wanaohusika.

Matamshi ya kamishna Ivuti yanalenga tu sio Kwale peke yake bali Pwani kwa ujumla, huku kaunti ya Mombasa ikionekana kuathiriwa zaidi na makundi hayo ya uhalifu, kama vile Wakali Kwanza na Wakali Wao.