Mbunge wa Mvita Adbulswamad Sharif Nassir ameisisitiza jamii ya pwani kudumisha amani, ushirikiano na utangamano haswa wakati huu taifa linapoelekea uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Akizungumza kwenye hafla ya kuchangisha pesa za kununua basi la kanisa katoliki la Makupa, Adbulswamad amesema kwamba haoni haja ya wakazi wa pwani kuanza kugombana na kuzua vurugu kwa misingi ya kikabila au dini.
Nassir ambaye alikuwa mgeni mheshimiwa katika hafla hiyo aliwataka waumini wa dini zote kueneza umoja na utangamano pasi na kusahau ushirikiano ili kaunti za pwani zipate maendeleo.
Akiandamana na wajumbe kadhaa kutoka afisini mwake, Nassir alisema kwamba viongozi wa kisiasa huchaguliwa na kila mtu pasi kuzingatia dini, kabila wala anakotoka mtu mradi tu sera zake ziwe na lengo la kuwafaidi wananchi wanaompa madaraka hayo.
Wakati uo huo kiongozi huyo amewataka wanasiasa wenzake kuacha siasa zinazoweza kuleta mgawamyiko miongoni mwa wakaazi wa pwani na badala yake kuwahimiza kuhubiri amani na utangamano.