Hivi karibuni shule za upili zimegeuka jahanamu.
Kila kuchao kuna shule ambayo inateketezwa na mali inayokadiriwa kuwa mamilioni ya pesa inaharibiwa kwa masaa machache.
Vitu vinavyoharibiwa vimechukua miongo kununuliwa na kujengwa, huku pia maisha yakihatarishwa.
Tumelaumu wadau wengi lakini tumesahau jukumu la dini.
Uislamu, Ukristo, Uhindi na utamaduni ni vyombo vinavyostahili kuleta utulivu katika jamii.
Nimetembea Kenya na nimeona asilimia ndogo sana ya shule zisizokua na uhusiano wowote na dini fulani.
Hata hivyo, kuna mipangilio ya ndani kwa ndani ya kuandaa vikao vya kidini katika shule hizo.
Hili linamaanisha kwamba hakuna shule isiyotangamana na uungu.
Ikiwa kuna mafunzo ya kidini, mbona utundu unapotosha wanetu?
Dini imesahau majukumu yake.
Nakumbuka enzi zetu ibada ilikua ni shughuli ya lazima. Kuanzia shule ya chekechea hadi upili, tulifunzwa kuheshimu wakubwa kwa wadogo.
Wale ambao wana mamlaka pia tuliambiwa wameteuliwa na Mungu.
Maimamu na kasisi walitupa mwelekeo wa kutamaniwa na jamii.
Visa vya utovu wa nidhamu vilikua lakini kiwango chake hakikuogofya kama tunavyoshuhudia siku hizi.
Tukilaumu waziri, walimu na wanafunzi, tusisahau dini.
Kuna ulegevu ambao sehemu hii ya jamii inastahili kuangazia.
Hili lisipofanyika tunapalilia kizazi cha majambazi sugu.