Wanaelewa vizuri kuwa kubeba mizigo kupita kiasi ni kuvunja sheria za barabarani.
Hii ni tabia ambayo imekuwa mtindo katika mji wa Kisii kwa wanabodaboda, huku Serikali ikizidi kupambana ili kupunguza ajali za barabarani ilhali wale wanaozitumia hawatilii maanani sheria hizo.
Mwanabodaboda huyu amenaswa katika barabara kuu ya Kisii-Kisumu hatua chache kutoka soko la Daraja Mbili akiwa amebeba mizigo inayozidi kiwango ambacho pikipiki inapaswaa kubeba.
Ukimtizama kwa makini, utagundua kuwa pikipiki yake inayumbayumba lakini yeye anakaza mwendo. Iwapo usalama utadumishwa barabarani, basi kwanza ni sharti mwanainchi mwenyewe binafsi aelewe kuwa kubeba mizigo kupita kiasi ni hatari.
Ni jukumu la kila Mkenya kuhakikisha kuwa gari analoliabiri halijabeba kupita kiasi na iwapo limebeba kupita kiasi, aelewe kuwa ana haki ya kupiga ripoti kwa polisi. Ni wakati ambapo mimi na wewe tunafaa kuchukua hatua. Usalama unaanza na wewe.
Kila mtu anasaka riziki lakini ni wakati wa kuelewa fika kuwa maisha ni muhimu. Wataalamu waliotengeneza pikipiki wametoa masharti wazi kuwa pikipiki inastahili kubeba abiria mmoja. Na pia imeundwa na kuwekewa kiwango cha mizigo ambacho inatakikana kubeba.
Kisii imeripotiwa kuhusika katika mikasa ya ajali za barabarani kwa siku chache zilizopita. Na hizi ni baadhi ya tabia ambazo huchangia kuongezeka kwa ajali barabarani. Kama dereva, abiria, mwanabodaboda ni wakati sote tushikane mikono na kusema hapana kwa tabia kama hizi.
Serikali wakiwemo maafisa wa trafiki hawana uwezo wa kuzuia ajali, ni mwanainchi binafsi kujiepusha. Tunaweza kujikinga kutokana na ajali kwa kuwa waangalifu kila tunaposafiri.