Wengi wa wasanii wa tasnia mbalimbali hupenda kuvalia mavazi ya nadhifu na yaliyo ghali ikilinganishwa na watu wa kawaida.
Takribani asilimia mia moja ya wasanii wa nyimbo pamoja na waigizaji hupenda kuvaa pete za dhahabu huku wengine wakipenda fedha (silver) kama ishara ya ukwasi walionao katika ulingo wa sanaa.
Yusuf Kombo, ni mmoja wa wasanii wanaotamba katika ukanda wa Pwani na Kenya nzima kwa jumla, huku kule Bungoma akiwa amewateka mashabiki wake kwa kiwango kisichodhamirika.
Barchelor Boy ndilo jina linalomfahamisha kwa wengine. Alijitosa ulingoni kwa jina Susumila na kuchukua nafasi rasmi kama mwimbaji maarufu na anayekula matunda baada ya kuvumilia mengi.
Susumila alizaliwa Chumani, Kaunti ya kilifi miaka 33 iliyopita na amekuwa kwenye tasnia ya muziki kwa miaka mingi sana.
Amekuwa mkali wa nyimbo na anakiri kuwa pete zake sio za kawaida kwani alitumia mkwanja mnene zifikazo elfu 38.
Alianza muziki mwaka wa 2000 na ngoma yake ya kwanza iliyompatia mafanikio mengi ni kibao cha Siasa Duni alichokitoa mwaka 2007, wimbo uliozungumzia maswala nyeti ya uongozi na wanasiasa.
Baada ya kutambulika, hakupumzika ila aliendeleza fani ya sanaa. Kufikia sasa, msanii Susumila ana nyimbo nyingi ambazo zingekua zinaekwa kwa mfumo wa album basi zingefika zaidi ya album nne.
Kollabo zake ambazo amefanya na wasanii mbalimbali hapa nchini ikiwemo Chikuzee na Kingkaka zimeendelea kumtambulisha katika ulingo wa sanaa kwa kiasi kikubwa.
Akiwa chini ya producer TK2 anayejulikana kwa kuwa mkali kanda ya Afrika Mashariki katika studio za Hornet, aliweza kupakua nyimbo kali ila baadae studio hizo zikasambaratika.
Kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wanaotiliwa gumzo mitandaoni na hata kwenye vyombo vya habari.