Tarehe moja mwezi Juni mwaka wa 1963 Kenya ilijipatia Uhuru na kujikomboa kutoka kwa serikali ya ukoloni na baadaye kupata uhuru kikamilifu mwezi Disemba tarehe 12 kutoka kwa serikali ya Uingereza.

Share news tips with us here at Hivisasa

Tarehe 1 mwezi Juni mwaka huu, Kenya itakua inaadhimisha miaka 53 ya kujitawala chini ya marais mbali mbali; Rais wakwanza wa Jamuhuri ya Kenya Jommo Kenyatta, Rais Daniel Arap Moi, Rais wa tatu Mwai Kibaki, na sasa chini ya uongozi wa Uhuru Kenyatta, rais wa nne wa Kenya.

Katika miaka yote hii, Kenya imepiga hatua mbali mbali ikiwemo kubuniwa kwa serikali za ugatuzi.

Japo yapo mengi ambayo Wakenya wengi wanajivunia, wengi wao hulalamika kuwa uchumi umezidi kudorora miaka 53 baada ya kupatikana kwa uhuru.

Waandishi wa habari kwa upande wao wanalalamika kuwa japo wamepiga hatua, zipo sheria nyingi ambazo zimepitishwa za kuwakandamiza.

Kwa muda mrefu sherehe kuu zimekua zikifanyika katika jiji la Nairobi lakini kinyume na miaka ya nyuma, sherehe za mwaka huu zitafanyika katika uwanja wa Afraha.

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto wataongoza hafla hizo mjini Nakuru.

Makamishna wa kaunti, katika kaunti zote 47, wataongoza sherehe hizo katika ngazi za kaunti zao pamoja na magavana.

Kaunti ya Mombasa itaanda sherehe hizo katika uwanja wa Tononoka ambazo zitaongozwa na kamishna mpya wa kaunti hiyo, Mohammed Maalim.

Maalim amesema kuwa mikakati kabambe imewekwa ili kuhakikisha kuwa sherehe hizo zinaendelea vyema.

Miaka 53 imepita lakini bado Kenya inakumbwa na changamoto tele hususan za kiuchumi, kiusalama na ajira.

Kupunguza umaskini pia imekua changamoto kuu.

Hata hivyo, wengi wanajivunia amani ambayo imedumu kwa muda mrefu nchini.

Yote tisa, kumi ni tujivunie kuwa Wakenya na kuendeleza uzalendo na kuwakumbuka mashujaa waliopigania uhuru unaoshuhudiwa sasa nchini.