Mrengo wa Cord umeishutumu vikali serikali ya Jubilee kwa madai ya kuhusika katika ufisadi, wizi wa mali ya umma na kuwa adui wa demokrasia.
Wakizungumza katika Kaunti ya Kwale katika mkutano wa kuwahimiza wakaazi kujisajili kama wapiga kura, viongozi hao wa upinzani, wakiongozwa na Raila Odinga, waliwataka Wakenya kuibandua madarakani serikali ya Jubilee katika uchaguzi ujao.
Raila alisema ni sharti Wakenya wajisajili kama wapiga kura kwa wingi, ili kuwa na fursa ya kuchagua viongozi bora mwezi Agosti.
“Jiandikisheni kwa wingi kama wapiga kura ili Jubilee isirudi madarakani,” alisema Raila.
Kiongozi huyo wa upinzani alidai kuwa Wakenya wengi wamebaki kuwa maskini kwa sababu pesa zao zinafujwa kila siku na viongozi wa Jubilee.
“Wakenya wanakufa njaa kwa sababu pesa zao zinaporwa kila siku na viongozi wa Jubilee,” alisema Raila.
Wakati huo huo, Raila alimshutumu Gavana Salim Mvurya kwa kujiunga na chama cha Jubilee, kauli iliyoungwa mkono na Gavana wa Kilifi Amason Kingi.