Vijana wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa masomo yanayopeanwa bila malipo na shirika la Microsoft mjini Nakuru.
Akiongea katika warsha ya vijana inayoendelea katika maktaba ya Nakuru chini ya shirika la Digital Opportunity Trust, Joseck Olala ambaye ni msimamizi wa zoezi hilo mjini Nakuru aliwaomba vijana kuchukua fursa hio ya kipekee kujinufaisha kimasomo.
“Ni karibu miezi mitatu sasa tangu tuanzishe mradi huu hapa Nakuru na ni wachache sana ambao wamejitokeza hadi sasa,” alisema Olala.
Shirika la Microsoft chini ya mradi ya Microsoft IT Academy linatoa fursa kwa wanafunzi na wakufunzi kote duniani kupata masomo ya utumizi wa tarakirishi bila malipo. Na kisha wanafunzi wapata vyeti ambavyo walithibitisha vinatambulika kote duniani.
“Baada ya kuhitimu, kila mwanafunzi anapata cheti ambacho ni dhibitisho kamili kwamba amafanya somo hili na cheti chenyewe kinakubalika popote duniani. Masomo pamoja na mtihani mtu binafsi ndiye anaamua wakati wa kuzifanya,” aliongeza Olala.
Ili kupata huduma hii, mwanafunzi anatakiwa kutembelea maktaba yoyote hapa nchini ili apate kujiandikisha na kupata akaunti yake ambayo atatumia kupata kila habari kuhusu masoma yote ya shirika la Microsoft IT Academy na kuweza kusomea popote bora awe na internet.
“Kwa wale ambao hawawezi kupata mtandao ama tarakilishi, KNLS inawaruhusu kutumia tarakilishi zao kila siku ya wiki bila malipo,” alimalizia Olala.