Mwanasiasa Evans Toel aliyewania kiti cha uakilishi wa Wadi ya Sensi ilioko katika eneo Bunge la Kitutu Chache Kaskazini, Kaunti ya Kisii amesema jina Sensi linastahili kubadilishwa kuwa Kitutu Central.
Akiongea mnamo siku ya Ijumaa kwenye mazishi ya mzee Amwoma Chweya yaliyoandaliwa katika kijiji cha Mosocho Nyakeri Lokesheni ya Mwamonari, Toel aliwaomba wakaazi wa Wadi hiyo kushirikiana naye kuomba tume ya Uchaguzi na mipaka nchini IEBC kulibadilisha jina hilo la Sensi kuwa Kitutu Central.
Mwanasiasa huyo aliyewania kiti hicho cha uakilishi wa Wadi mwaka wa 2013 alisema jina hilo la Sensi linawatatisha watu wengi kuelewa ni Wadi ipi maana eneo la Mwamonari na eneo la Sensi yaliunganishwa pamoja.
“Nataka jina hili libadilishwe na tume ya uchaguzi nchini ili Wadi hii iwe ikiitwa Kitutu Central maana wakaazi wengi hushindwa kubaini ni wa eneo la Sensi au ni wa eneo la Mwamonari,” alisema Toel.
Wakati uo huo, wakaazi wa eneo hilo walionekana kufurahishwa na ombi la mwanasiasa huyo na kusema sharti jina hilo liwe limebadilishwa kabla ya mwaka wa 2017 wakati uchaguzi mwingine utafanywa nchini.
“Tutafurahia sana jina hilo likibadilishwa na pia tunamwomba Mwakilishi wa Wadi hii Ochong’a Nyagaka kuunga mkono ombi hilo ili jina hili libadilishwe kuwa Kitutu Centra,” alihoji Geoffrey Omori mmoja wa wakaazi wa Wadi hiyo ya Sensi.
Kibarua sasa ni kwa Mwakilishi aliye kwenye kiti hicho cha uakilishi wa Wadi hiyo ya Sensi Nyagaka kushirikiana na mwanasiasa Toel pamoja na wakaazi wa Wadi hiyo kuhakikisha jina hilo limebadilishwa kabla ya uchaguzi ujao.