Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu kaunti kamishna katika kaunti ndogo ya Nakuru Magharibi (DCC) Elmi Shaffi Ibrahim, ametoa tetsi kwamba baadhi ya vijana wanaokaa katika eneo maarufu kama Jobless Corner wilayani humo, hushiriki uhalifu.

Ni kutokana na hilo ambapo mkuu huyo mpya amesema: “Sasa eneo hilo litakuwa ofisi yangu, hakuna tena kitu kama Jobless Corner, kwa sababu nitatuma chifu awe akifanyia kazi eneo hilo na kwa hivyo biashara haramu itaisha”

Akizungumza katika eneo la Mwariki Ijumaa baada ya kuongoza maafisa wa Polisi wa Utawala (AP) kuharibu zaidi ya pombe haramu lita 5,000; Shaffi alikariri kwamba eneo hilo la Jobless Corner limetambuliwa na maafisa wa polisi kama kitovu cha kuvutia bangi na uuzaji wa mihadarati miongoni mwa vijana.

“Afadhali mtu aachane na hiyo biashara kwa sababu sitakomesha misako hii, nitaifanya hata kama ni siku kuu, wikendi ama siku nyingine yeyote ile,” alisisitiza.

Alisema kwamba serikali inajikakamua kusaidia vijana walioadhirika na pombe haramu pamoja na dawa za kulevya kupata usaidizi wa kurekebisha tabia.

“Changamoto kubwa kwetu katika kukabili pombe haramu; ni wauzaji wa molasses. Pia wafanyibiashara laghai wa pombe haramu wamegundua mbinu mpya za kuificha, hivi kwamba maafisa wa polisi hawawezi kugundua” akasema bwana Shafi, akitoa mfano na mshukiwa Muriuki ambaye alikuwa amechimba shimo kubwa kando ya nyumba yake, lenye uwezo wa kuhifadhi maelfu ya lita za pombe haramu.