Gavana wa Mombasa Hassan Joho ameagizwa kufika katika kituo cha polisi cha Malindi kuandikisha taarifa kuhusiana na vurugu zilizoshuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa Malindi uliofanyika Machi 7.
Kwenye mtandao wake wa Twitter na Facebook siku ya Jumatatu usiku, Joho alithibitisha kupokea simu kutoka kwa wizara ya usalama kuandikisha taarifa kwa idara ya usalama hii leo saa nne kuhusiana na vurugu hizo.
Hata hivyo Joho amesema kuwa hatoweza kufika katika kituo hicho hadi siku ya Alhamisi kwa kuwa ana majukumu ya kikatiba anayohitaji kutekeleza kwa wananchi wa kaunti ya Mombasa.
Kando na Joho, wabunge wote wa upinzani kutoka eneo la Pwani vile vile wametakiwa kufika kwenye kituo cha polisi cha Malindi kuandikisha taarifa.
Haya yanajiri wiki moja tu baada ya Joho na waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery kutofautiana kuhusu umiliki wa bunduki ambapo Gavana huyo alitakiwa kusalimisha bundiki anayomiliki kwa idara ya usalama.