Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ameahidi kuweka juhudi zaidi kwenye serikali yake ili kuona kuwa idara ya afya inaimarika zaidi na kila mkazi wa kaunti hiyo anapata afya bora na huduma za kuridhisha.
Joho amesema kuwa serikali yake iko tayari kushirikiana na watu binafsi pamoja na mashirika mbali mbali kama yale ya kijamii pamoja na mashirika mengine ambayo huakikisha kuwa wakazi wanapata kuimarika kiafya.
Akiongea siku ya Jumamosi katika hafla moja ya kupokea ufadhili wa vifaa vya hospitali kuu ya rufaa ya Coast mjini Mombasa, Joho aliwataka viongozi wengine pamoja na mashirika kutoka kaunti ya Mombasa kuendelea kuonyesha roho ya kufadhili miradi mbali mbali pamoja na kuiona kuwa sekta ya afya inaboreshwa zaidi.
Joho ambaye alikuwa mgeni alikwa kwenye hafla kiyo ambayo ilishuhudia kutolewa kwa zaidi ya vitanda 200, mablanketi, vitanda vya wajawazito na vifaa vingine na mfadhili mmoja ambaye ni mkazi wa jiji la Mombasa, aliwataka wakazi wengine kufuata mfano kama wa mfadhili huyo na kudokeza kuwa serikali yake itaweka mikakati kamili ya kupandisha viwango vya huduma vinavyotolewa katika hospitali hiyo ambayo ndio kubwa miongoni mwa hospitali za umma katika eneo zima la pwani.
Kwa upande wake, mfadhili wa vifaa hivyo, Bw Ahmed Al-Falesi alisema kuwa ni furaha yake kuona huduma za hospitali zikiwa bora kwa wakazi ambapo aliahidi kuendelea kufadhili miradi mingine ya ziada kwenye kaunti hiyo.