Mgogoro kuhusiana na mradi wa nyumba za makaazi unaonuiwa kutekelezwa na serikali ya Kaunti ya Mombasa unatarajiwa kuchacha hata zaidi baada ya Gavana Hassan Joho kushikilia kwamba mradi huo utatekelezwa kikamilifu kulingana na mpangilio uliopo.
Kauli ya Joho inajiri baada ya mwanasiasa Suleiman Shahbal kusisitiza kwamba iwapo mradi huo hautasitishwa na wakaazi kuhusishwa kikamilifu, basi atawaongoza wakaazi hao kuishtaki serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kuutekeleza mradi huo kinyume cha sheria.
Joho alisema kwamba mradi huo wa shilingi bilioni 200 utasaidia katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za makaazi katika kaunti hiyo ya Mombasa.
Hatahivyo, alilalamika na kusema kwamba mradi huo tayari umeingizwa siasa bila ya wanasiasa hao kutambua umuhimu wake.
Akizungumza katika eneo la Majengo mjini Mombasa siku ya Jumanne, gavana huyo alisema kwamba uhaba huo wa nyumba za makaazi katika kaunti hiyo umesababisha kuzuka kwa mitaa ya mabanda, misongamano ya nyumba, na ukosefu wa mpangilio wa jiji la Mombasa.
"Serikali ya Kaunti ya Mombasa itatekeleza mradi huo hata kama wale jamaa wengine wataingiza siasa kwa sababu wakaazi wa Mombasa ndio wanaopitia changamoto ya kuishi katika hali duni. Iwapo hatutawaboreshea makaazi watu wetu, watazidi kuteseka na ndio maana tunasema lazima mradi huo kutekelezwa kikamilifu,” alisema Joho.
Juma lililopita, malumbano yalichacha kati ya serikali ya kaunti na wakaazi wanaoishi kwenye nyumba za umma baada ya wakaazi hao kutakiwa kuzihama nyumba hizo, ili kupisha ujenzi wa nyumba mpya.