Wachangauzi wa maswala ya kisiasa katika eneo la Pwani wamesema kuwa Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho pamoja na viongozi wengine walioagizwa na afisa wa usajili wa silaha kurudisha bunduki zao kwa idara ya polisi wanafaa kufanya hivyo kuzuia kushuhudiwa kwa migogoro ya kisiasa Pwani.
Wakiongozwa na Wakili Johnson Muchiri, wachanganuzi hao walisema kuwa kila kiongozi anafaa kupewa ulinzi sawia na viongozi wengine kwa mujibu wa katiba, lakini iwapo idara ya usalama imegiza walinzi hao kuondolewa, sharti viongozi hao watii agizo hilo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Muchiri alisema kuwa malumbana ya kila uchao na kuonyeshana ubabe wa kisiasa kunachangia kudidimia kwa maswala muhimu ya kimaendeleo katika Kaunti ya Mombasa na eneo zima la Pwani.
Mchanganuzi huyo wa maswala ya kisiasa alishikilia kuwa vita vya serikali na mwananchi ni vita vigumu sana na iwapo viongozi watazidi kukaidi agizo hilo, huenda eneo la Pwani likashughudia mgogoro mkubwa ambao utaathiri pakubwa maswala ya uwekezaji, uchumi na hata kuzorotesha sekta ya utalii ambayo imeanza kuimarika.
"Tunasema kuwa ni vyema viongozi walioagizwa kurudisha silaha zao kufanya hivyo ili kuzuia eneo hili kuwa na migogoro kwa sababu iwapo wataendelea kujifanya hao ni viongozi bora, basi vita vya serikali na baadhi ya watu fulani vitakuwa vigumu sana. Wasifikirie kuwa Wakenya watawaunga mkono. Watu wamechoka na kusukumwa kila siku kwa mambo yasiokuwa na umuhimu,” alisema Muchiri.