Gavana wa Mombasa Hassan Joho amesema kuwa serikali ya kitaifa sharti ikabili wafisadi katika wizara mbalimbali ili kuhakikishia wananchi ugavi sawa wa rasilimali.
Joho alisema kuwa iwapo serikali ya kitaifa itaendelea kuwatetea wafisadi, wananchi wataendelea kuhangaika.
Akizungumza mjini Mombasa, Joho alinyoshea kidole cha lawama serikali ya Jubilee kwa kushindwa kukabiliana vilivyo na jinamizi la ufisadi, hali aliyosema imepelekea Wakenya kukosa huduma muhimu.
Joho alisema bila ya jinamizi la ufisadi kuangaziwa kikamilifu na wahusika kukabiliwa kisheria, basi taifa hili litazidi kurudi nyuma kiuchumi na kimaendeleo, huku mali ya umma ikizidi kuwanufaisha wachache.
“Serikali ya Jubilee imezongwa na ufisadi na ni lazima wakabiliane nalo ili tupate ugavi sawa wa rasilimali kwa wananchi,” alisema Joho.
Aidha, Joho aliikosoa Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, kwa kushindwa kuthibiti visa vya ufisadi nchini.
Wakati huo huo, Joho amewataka wakaazi kuwa mstari wa mbele kufichua ufisadi katika ngazi mbali mbali wanapozuru afisi za serikali, ili kuhakikisha wahusika wanakabiliwa na mkono wa sheria.