Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho ameishambulia serikali ya Jubilee na kusema kuwa imeshindwa katika kuyatekeleza majukumu yake tangu iingie mamlakani.
Joho amesema kuwa vinara wakuu wa Jubilee; Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kamwe hawajatimiza ahadi walizoahidi kwa Wakenya wakati alipoapishwa yapata miaka mitatu sasa.
Akiwahutubia wakaazi wa mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Joho alisema kuwa Uhuru na Ruto wamekuwa wakizunguka katika sehemu mbalimbali nchini wakieneza sera ambazo kamwe hazilengi kubadilisha maisha ya Mkenya, na akahoji kuwa Jubilee imeshindwa kumuwajibikia Mkenya.
Joho amewataka viongozi wa Jubilee kuheshimu upinzani unaoangania maslahi ya Wakenya mashinani na wala sio kuwakejeli.
"Tunakosa kuelewa hii serikali ya Jubilee jinsi inavyofanya kazi kwani imedhihirisha wazi kuwa imeshindwa kuwajibikia majukumu yake na pia waheshimu mrengo wa Cord kwa sababu Cord ni chama cha kutetea maslahi ya munyonge," alisema Joho.
Kauli ya Joho inajiri huku Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto wakikamilisha ziara yao ya siku tatu katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi.