Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amependekeza serikali kuu kupunguzia kaunti hiyo mgao wa fedha za bajeti, na kutumia fedha hizo kugharamia hati miliki za wakaazi wa Shamba la Waitiki katika eneo la Likoni.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiwahutubia wakaazi wa eneo la Mikindani katika hafla ya kutoa vifaa ya matibabu kwa Zahanati ya Mikindani mjini Mombasa siku ya Jumatano, Joho alisema kuwa sio vyema kwa serikali kuwaitisha wakaazi wasio kuwa na uwezo wa kujimudu kimaisha pesa.

Joho alisema kuwa shilingi elfu 182 kwa kila mmiliki wa kipande cha ardhi ni ada ya juu zaidi ikilinganisha na hali ngumu ya maisha ya sasa.

Aliisuta serikali ya Jubilee kwa kudai kuwa inachangia maisha magumu kwa wakaazi wa mashinani.

"Kama Serikali ya Kaunti ya Mombasa, tuko tayari kwa serikali kuu kutupunguzia mgao wa fedha za bajeti mradi wakaazi wetu wa Shamba la Waitiki wasilipe ada yoyote. Wachukue zile zao na zingine watupe na wala sisi watu wa Mombasa hatutalalamika,” alisema Joho.

Kauli ya Joho imejiri baada ya wakaazi wa Shamba la Waitiki kulalamika kuwa hawana fedha za kulipa ada ya shilingi elfu 182.