Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amekana madai kuwa ana ushawishi katika vurugu za kila mara zinazoshuhudiwa katika bunge la kaunti hiyo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwenye mahojiano ya simu na stesheni moja ya redio mjini Mombasa siku ya Jumanne, Joho ambaye anadaiwa kuunga mkono pande moja kati ya pande mbili zinazozozana, alijitenga na purukushani hizo.

“Vurugu hizo zimenipata kwa mshangao. Sifahamu vyema mgogoro huo unasababishwa na nini wala sielewi mbona wabunge wa kaunti wanashinda wakizozona,” alisema Joho.

Aidha, Joho ameitaka idara ya usalama kuingilia kati na kufanya uchunguzi ili kubaini kiini cha mvurutano huo, ambao ameutaja kama kikwazo kwa maendeleo ya kaunti.

Gavana huyo alisema kuwa vurugu hizo zimelemaza shughuli za bunge hilo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

“Itakuwa vyema kwa maafisa wa usalama kuingilia kati sasa maana hali inayoshuhudiwa katika bunge hilo inazamisha shughuli za kaunti wala haileti picha nzuri kwa wakaazi wa Mombasa,” aliongeza Joho.

Kauli ya Joho inajiri baada ya karatasi zilizosambazwa zikiwatishia Spika Thadiaus Rajuwayi na kiongozi wa wengi Abdalla Kasagamba kumhusisha Gavana Joho na mvutano huo.