Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amelikashifu tukio la siku ya Jumatatu ambapo viongozi wa Cord walirushiwa vitoa machozi na maafisa wa usalama walipokuwa wakiandamana kuelekea katika afisi za Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka nchini IEBC.

Kwenye mtandao wake wa Facebook, Joho alieleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo huku akiitaja kama utumiaji vibaya wa mamlaka na ukandamizaji wa uhuru na demokrasia ya viongozi wa upinzani.

“Ni jambo lisilokubalika hata kikatiba. Sheria yetu imetoa nafasi kwa kila mtu kuandaa maandamano ya amani. Iweje viongozi wa Cord wanasambuliwa kwa kurushiwa vitoa machozji,” alisema Joho.

Aidha, Joho alisisitiza kuwa sharti tume ya IEBC ibanduliwa kabla uchaguzi mkuu wa mwaka ujao kwani Wakenya tayari wameonyesha kutokuwa na imani nayo, kutokana na namna ambavyo imekuwa ikiendesha shughuli zake.

Siku ya Jumatatu, vinara wa Cord wakiongozwa na Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula walirushiwa vitoa machozi na maafisa wa polisi walipokuwa wakiandamana keulekea afisi za IEBC kwa lengo la kuwatimua maafisa wa tume hiyo.

Hata hivyo, viongozi hao wameapa kuendelea na shinikizo hizo hadi tume ya IEBC itakapobanduliwa.