Mbunge wa Nyali Hezron Awiti amemshutumu Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho, kwa madai ya kuchochea wakaazi wa eneo hilo dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa.
Awiti alidai kuwa Joho amekuwa akiwataja wapinzani wake kama wabara ambao hawana nafasi katika siasa za ukanda wa Pwani.
"Ni jambo la kusikitisha kwa gavana kudai kwamba wakaazi wazawa wa Pwani ndio wanaofaa kujitosa katika siasa za kaunti. Madai kama hayo hayana msingi wowote na hayafai,” alisema Awiti.
Mbunge huyo wa Nyali alisema kuwa Mombasa ni moja ya miji iliyo na wakaazi wa tamaduni mbalimbali, na kuongeza kuwa nyadhifa za uongozi zapaswa kuwa wazi kwa watu kutoka sehemu yoyote ya nchi kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Awiti pia alimtaka gavana huyo kueleza ni kwa nini familia zilizo na ushawishi mkubwa katika eneo la Pwani, ndizo zinazomiliki vipande vikubwa vya ardhi ilhali wakaazi wanaendelea kuishi kama maskwota katika ardhi zao.
Awiti ametangaza hadharani azma yake ya kumuondoa Gavana Joho madarakani katika uchaguzi mkuu ujao, kwa kusema kuwa kanda ya Pwani inapaswa kurejeshewa utukufu wake.