Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amepuuzilia mbali matamshi ya Naibu Rais William Ruto ya kumtaja kama mchache wa elimu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza katika mkutano na wananchi katika kaunti ndogo ya Jomvu, Joho alisema kauli ya Ruto ya kusema hana ufahamu na maswala ya bandari haina msingi wowote, ikizingatiwa kuwa amekuwa akiishi na kutekeleza biashara zake katika bandari hiyo.

“Hauwezi nifunza mambo ya bandari kwa sababu naishi katika maeneo haya, labda unifunze ukulima,” alisema Joho.

Joho alisisitiza kuwa kamwe hatosita kuwatetea wananchi wake dhidi ya hujma za serikali ya kitaifa.

“Kama kutetea watu wangu ni kukosa elimu, sawa wacha niikose lakini dhulma dhidi ya watu sitokubali,” alisema Joho.

Alisema kuwa baadhi ya viongozi katika serikali kuu wamekuwa wakieneza propaganda zisizokuwa na msingi wowote, jambo ambalo amelitaja kama la kuwapotosha wananchi.

Joho aliukosoa mpango wa kuweka Bandari ya Mombasa chini ya serikali kuu, na kusisitiza kuwa hatua hiyo inapania kuhujumu wakaazi wa Mombasa wanaotegemea bandari hiyo pakubwa.

Alisema kuwa mpango huo utakosesha idadi kubwa ya vijana na wakaazi wa Mombasa ajira na hatimaye kuongeza viwango vya umaskini.