Gavana wa Mombasa ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM amelaani kitendo cha polisi kuwacharaza viboko wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi siku ya Jumatatu.
Kwa sasa chama hicho cha ODM kinasema kuwa kinahitaji maelezo kamili kutoka kwa wizara ya usalama wa ndani kuhusu kitendo hicho cha ahibu kutoka kwa polisi.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne, Joho alisema kitendo cha polisi kutumia nguvu wakati wa kudhibiti fujo ni kinyume cha sheria na ishara wazi kwamba hawajui majukumu yao.
“Kulingana na katiba mpya polisi hana sababu ya kumpiga mwanafunzi wakati wa maandamano bali wanafaa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka,” Alisema Joho.
Kiongozi huyo anaongeza kuwa wanashangazwa na jinsi serikali kuu imewapa askari wa kawaida mamlka ya juu jambo linalowafanya kuvuka mipaka wanapokuwa kazini.
Wakati huo huo gavana Joho alisisitiza kuwa serikali ya Jubilee inafaa kuhakikisha inajenga imani baina ya polisi na wananchi kulingana na katiba ya nchi.
“Watoto wetu katika vyuo vikuu hawafai kuchukuliwa kama maadui, hivyo ndivyo walifanya Nairobi na waziri wa usalama wa ndani anafaa kujukumika,” aliongeza Joho.
Kauli ya Joho inatokana na kitendo cha askari kuwacharaza wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi siku ya Jumatatu walipokuwa wakiandamana kupinga uchaguzi wa Babu Owino kama Rais wa muungano wa vyuo vikuu.