Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho ametakiwa kumrudishia katibu wa kaunti Francis Thoya, mamlaka ya mkuu wa Idara ya Ardhi, Makao na Mpangilio wa Mji.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Shirika la ardhi la ‘Residents Land Protection Organisation of Kenya’ limekosoa mabadiliko hayo na kusema kwamba Thoya alikuwa ameliwajibikia swala la ardhi katika Kaunti hiyo ya Mombasa na tayari migogoro mingi ya ardhi ilikuwa imeanza kutatuliwa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mwenyekiti wa shirika hilo nchini Dewelly Nyambu alisema kwamba Thoya alizuru mashinani na kukutana na jamii hasa katika maeneo ya Mwakirunge, Nguu tatu, Mtopanga na hata Changamwe kunakozongwa na migororo mingi ya ardhi.

Nyambu alisema kuwa Thoya pia alikuwa amefika mahakamani ili kuwatetea wakaazi wapate ardhi zao.

Nyambu alisema kwamba punde tu baada ya Thoya kubadilishiwa mamlaka na kuwa Katibu wa serikali ya Kaunti ya Mombasa, wakaazi wameanza kuhangaishwa na kupewa ilani ya kuzihama ardhi zinazokumbwa na migogoro huku baadhi yao wakichomewa nyumba zao za makaazi.

"Tunamtaka Gavana Joho kuangalia kwa kina swala hili kwani Thoya alikuwa akiwajibikia majukumu yake. Alifika nyanjani kuonana na wakaazi kuhusu swala la unyakuzi wa ardhi na kwa kiasi kikubwa swala hilo lilikuwa limeanza kupata suluhu. Wakaazi wengi walikuwa wanaishi kwa amani lakini sasa wameanza kufurushwa tena,” alisema Nyambu.

Mapema mwaka huu, Gavana Joho alilifanyia baraza lake la mawaziri mabadiliko ambapo Thoya, aliyekuwa mkuu wa Idara ya Ardhi alipandishwa hadhi hadi wadhifa wa katibu wa serikali.