Mahakama kuu imetoa agizo la kumzuia waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery kumkamata Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho pamoja na kutochukua bunduki anazomiliki.
Katika uamuzi uliotolewa na jaji wa mahakama hiyo George Odunga jijini Nairobi, seneta wa Siaya James Orengo akimwakilisha Gavana Joho alisema kuwa Nkaissery hakuwa na mamlaka ya kutoa agizo la kufutiliwa mbali kwa leseni ya kumiliki bunduki kwa gavana huyo.
Siku ya Jumanne, Joho alikwenda mahakamani kupinga agizo lilitolewa na Nkasseiry pamoja na makataa ya hadi Jumanne saa nane mchana kuwasilisha bunduki zake ama kukamatwa.
Hapo awali, Joho alisema kuwa haogopi kutiwa mbaroni na kufungwa gerezani baada ya kukaidi amri ya kuwasilisha bunduki anazomiliki kwa polisi.
Joho amemtaka waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkasseiry kutomtishia kuwa atatuma watu kumkamata akisema kuwa pindi tu watakapoamua kumtia mbaroni atawaeleza mahali pa kumpata na kutekeleza agizo hilo.
Kesi hiyo itasikilizwa Aprili 8,2016.
Picha: Gavana wa Mombasa Hassan Joho. Alienda mahakamani kusimamisha agizo la waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaiserry la kutaka kumta mbaroni. Maktba