Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amepiga marufuku utupaji wa taka katika jaa la Kibarani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Joho alisema kuwa hatua hiyo inanuia kuboresha mazingira safi ya mji wa Mombasa, huku akiongeza kuwa tayari shughuli ya uboreshaji wa eneo hilo imeanza.

Joho alisema kuwa mji wa Mombasa ni kitovu cha utalii na kushuhudiwa kwa mirindiko ya taka katika eneo la Kibarani, kutaharibu uchumi wa eneo hilo.

Joho alisema kuwa huenda wawekezaji wengi wakasusia kuekeza katika Kaunti ya Mombasa, kufuatia mazingira hayo duni.

"Kwa vile serikali ya kaunti inajali maslahi ya wananchi wake, tumesitisha utupaji wa taka katika jaa la Kibarani ili eneo lile lifanyiwe ukarabati, kama njia moja ya kuimarisha mazingira yetu,” alisema Joho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mazingira Kaunti ya Mombasa Tendai Lewa alisema kuwa jukumu hilo limo mikononi kwa serikali ya kaunti, itakayo hakikisha kuwa wakaazi wa Mombasa wanapata mazingira safi.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Mamlaka ya Baharini nchini KMA, kwa ushirikiano na mashirika ya kimazingira kutoa ilani ya siku saba kutolewa kwa taka katika eneo la Kibarani.