Gavana wa Mombasa Hassan Joho ameipongeza hatua iliyochukuliwa na serikali kuwaalika viongozi wa upinzani katika Ikulu ya Rais jijini Nairobi.
Akizungumza siku ya Jumatano katika uwanja wa Tononoka, Kaunti ya Mombasa, wakati wa maadhimisho ya siku ya Madaraka, Joho alisema kuwa mazungumzo baina ya serikali na viongozi wa upinzani ndiyo njia ya kipekee ya kudumisha amani katika taifa hili.
Aidha, alisema kwamba hatua ya viongozi wa Cord kutohudhuria hafla hiyo ya kitaifa iliyoandaliwa katika Kaunti ya Nakuru haimanishi kuwa hawatahudhuria majadaliano kuhusu Tume ya IEBC.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna mpya wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed alisema kuwa wako tayari kukabiliana na visa vyovyote vya uhalifu haswa wakati wa sherehe za mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Aliwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kuripoti mtu yeyote wanayemshuku kuwa mhalifu.