Gavana wa Mombasa.Hassan Joho.Awali.[Picha/kenya-today.com]

Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Mombasa Hassan Joho pamoja na wafanyikazi wengine wa kaunti hiyo wametakiwa kujiuzulu baada ya kuibuka madai ya ufisadi ndani ya serikali ya kaunti ya Mombasa.

Kauli hiyo ya kujiuzulu imetolewa na Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika,ambalo limemtaka gavana huyo kuondoka madarakani mara moja kwa kushindwa kuzuia ufisadi.

Mkurugenzi wa Haki Afrika, Hussein Khalid amesema kuwa gavana Joho ameshindwa kupambana na ufisadi uliokithiri ndani ya serikali ya kaunti ya Mombasa.

“Joho hafai kuwa madarakani kama ameshindwa kumaliza ufisadi unaohusishwa na serikali yake,anafaa ajiuzulu mara moja”,alisema Khalid.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili, Khalid amewataka wale wote walihusika na ufujaji wa fedha za umma katika serikali ya kaunti ya Mombasa kuchukuliwa hatua za kisheria .

“Kuna wafanyikazi wengine ndani ya serikali ya Joho,pia wanafaa kujiuzulu,wao pia wanajihusisha na ufisadi huo”,alisema Khalid.

Amemtaka Joho na wenzake kujiuzulu ili uchunguzi dhidi yao kufanywa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Watoke madarakani,ili uchunguzi dhidi yao kuanza mara moja na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao”,alisema Khalid.

Kauli hii inajiri  baada ya ripoti ya mhasibu mkuu wa pesa za umma nchini Edward Auko kufichua kuwa kaunti ya Mombasa imepoteza takriban billion 7.4 kwa njia ya ufisadi.

Kaunti ya Mombasa ni moja wapo ya kaunti zilizotajwa kuhusika katika ufujaji wa fedha za umma kulingana na ripoti ya mkaguzi mkuu nchini.