Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM ametoa rambirambi kwa familia ya Stephen Mukabana aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa Jumanne.

Mukabana aliyekuwa kiongozi wa vijana katika chama cha ODM tawi la Nairobi alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika makaazi yake eneo la Kayole mjini Nairobi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano, gavana Joho alimtaja Stephen kama kijana mwanaharakati na kutaja kifo chake kama pigo kwa chama hicho.

“Nimemjua Stephen kama kijana jasiri na mwanachama mkweli wa ODM, ningependa kutoa rambirambi zangu kwa familia na chama cha ODM kwa ujumla,” alisema Joho.

Joho alisema kuwa anamkumbuka zaidi kijana huyo kutokana na juhudi zake za kuwahimiza vijana wenzake kutafuta vitambulisho na kujiandikisha kama wapiga kura.

Wakati uo huo kiongozi huyo wa ODM alisema kuwa chama hicho kitafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa uchunguzi unafanywa kuhusiana na mauaji hayo ya kinyama.

“Tutahakikisha kuwa tunashinika uchunguzi na pia tunataka kuona kwamba waliohusika na kitendo hicho wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka,” aliongeza Joho.