Gavana Hassan Joho amewahimiza wakaazi wa Mombasa kuhudhuria vikao vya kujadili miradi ya maendeleo ambavyo vilianzishwa katika sehemu mbalimbali za kaunti.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Gavana Joho alisema kuwa ni haki ya mwananchi kuhusishwa kwenye miradi yoyote ambayo serikali inapania kuanzisha.
Alisema kuwa kama njia mojawapo ya kuheshimu katiba serikali ya kaunti kupitia kwa idara mbalimbali itaanza kuandaa vikao hivyo, ili kuhakikisha wakaazi wanahusika kikamilifu katika kujadili miradi hiyo.
Kulingana na Joho, vikao hivyo vitaandaliwa kila siku ya Jumanne katika maeneo bunge yote sita yanayojumuisha Kaunti ya Mombasa.
Joho alisema kuwa kikao cha kwanza kitakuwa katika eneo bunge la Mvita tarehe Septemba 6 katika ukumbi wa baraza, kisha baadae eneo bunge la Changamwe litafuata, kisha Jomvu, Kisauni, Nyali na kumalizia na eneo bunge la Likoni.
Joho alisema kuwa mawaziri wa serikali yake watakuwa na jukumu la kuongoza vikao hivyo ambapo watawaelezea wananchi kuhusu miradi hiyo na kusikiza maoni yao, kisha kutoa majibu kwa maswali ambayo yataibuliwa na wananchi.
Haya yanajiri baada ya Seneta wa Mombasa Hassan Omar kuibua maswali tata kuhusiana na matumizi ya fedha za bajeti ya kaunti.
Joho amesema kuwa mawaziri hao watajumuisha maoni ya wakaazi na kisha kuamua ni miradi ipi ambayo serikali ya kaunti itaangazia.