Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewaonya maafisa wa kaunti wenye tabia ya kuchukua hongo kutoka kwa wakaazi kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria iwapo watapatikana na hatia.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri baada ya jamaa mmoja kuripoti kuwa kwa muda sasa baadhi ya maafisa hao wamekuwa wakichukua rushwa kutoka kwake kila siku.

Joho alimruhusu jamaa huyo kwa jina Peter Oluoch kutoka eneo la Vipingo Ridge mjini Mombasa, kuwakagua maafisa hao afisini mwake mmoja baada ya mwingine ili kuwafichua wahusika.

Hatua hiyo ilipelekea maafisa wawili kuachishwa kazi baada ya jamaa huyo kufanikiwa kuwatambua, huku Gavana Joho akionya kuwa maafisa wengine watatumwa nyumbani hivi karibuni ikiwa hawatakoma kujihusisha na visa vya ulaji rushwa.

“Tabia hii lazima ikome. Tumekuajiri, tunakulipa na bado unachukua hongo kutoka kwa wananchi. Kuanzia leo ukipatikana, ujue nafasi yako itapewa mwingine mwenye yuko tayari kuwahudumia wananchi,” alisema Joho.

Aidha, Joho aliwahimiza wakaazi mjini humo kuripoti visa vyovyote vya ufisadi kwa idara ya kuanti inayopambana na ufisadi kupitia mtandao wa ethics@mombasa.go.ke.

Wakaazi mjini Mombasa kwa muda sasa wamekuwa wakilalamikia kulazimishwa kutoa hongo na maafisa wa jiji hasa akina mama wanaofanya biashara ya kuuza matunda na vyakula.