Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewaonya makamishna nchini dhidi ya kutumika kama mawakala wa chama cha Jubilee.
Joho amewahimiza makamishna hao kuwajibika katika utendakazi wao na kuwahudumia wananchi kama inavyostahili.
Joho alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwaona baadhi ya makamishna wakipigia debe chama cha Jubilee.
Akizungumza wakati wa sherehe za Jamhuri zilizoandaliwa katika uga wa Tononoka mjini Mombasa, Joho alionekana kutounga mkono hatua ya baadhi ya makamishna kujihusisha na maswala ya kisiasa huku wakitekeleza majukumu yao.
“Mambo na siasa, tuachieni sisi wanasiasa. Jukumu lenu ni kuhakikisha kuwa maswala ya usalama na amani yanatekelezwa mijini,”alisema Joho.
Joho alisema kuwa desturi hiyo ya makamishna kujihusisha na maswala ya siasa ni ya kutamausha haswa ikizingatiwa kuwa ukakamavu unahitajika pakubwa katika kuimarisha usalama, haswa msimu huu wa likizo.
Aidha, amewataka wanasiasa kuhubiri jumbe za amani wanapohutubia majukwaa ili kuepuka vurugu.