Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amelionya bunge la Kaunti ya Mombasa dhidi ya kufarakana na kuzabana makonde hadharani, akisema kuwa hatua hiyo sio ya nidhamu.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Joho alisema kuwa tabia hiyo ni kinyume na maadili.
Joho alisema kuwa viongozi wanapaswa kujadili maswala muhimu ya kimaendeleo pamoja na kuangazia maswala yatakayoboresha huduma kwa wakaazi wa kaunti hiyo.
Kiongozi huyo wa kaunti alisema kuwa ni aibu kubwa kwa wawakilishi wadi kupigana kwa misingi ya kisiasa, hali aliyosema inatoa taswira mbaya kwa wakaazi.
Aidha, alisema kuwa hatua hiyo inaonyesha kuwa bunge hilo limeshindwa kuyatekeleza majukumu yake kikamilifu.
Gavana Joho aliwatahadharisha wawakilishi hao wa wadi dhidi ya kuonyesha upotovu wa maadili pindi wanapokuwa bungeni.
"Ni lazima muafikiane iwapo kuna tofauti zozote kuhusiana na utenda kazi wenu na wala sio kuendeleza upuzi mbele ya wakaazi wa kaunti ya Mombasa. Hiyo sio sawa kama kiongozi,” alisema Joho.
Haya yanajiri baada ya wawakilishi wadi hao kuzabana makonde hadharani baada ya baadhi yao kutaka kumuondoa mamlakani Spika Thadius Rajwayi.