Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa kaunti ya Mombasa sasa wana matumaini baada ya gavana wa kaunti hiyo Ali Joho kutangaza kuwa hospitali zote za umma eneo hilo ziwaachie huru wagonjwa wote waliozuiliwa kutokana na madeni.

Hii ni baada ya gavana huyo kugundua kwamba kuna familia nyingi zinazopitia hali ngumu ya maisha baada ya wapendwa wao kuzuiliwa kwa muda mrefu hospitalini hadi pale watakapokamilisha madeni hayo.

Akiongea wakati wa sherehe za Jamhuri mjini Mombasa siku ya Jumamosi, joho alisema kuwa hiyo ndio zawadi ya kipekee angependa kuwapa wakaazi wa kaunti yake wakati huu taifa linaposherehekea.

“Kama kuna mgonjwa leo hii mabaye amezuiliwa hospitalini na ni maskini nasema apewe uhuru wake wakati tunaposherehekea Jamhuri,” alisema Joho.

Bi Zainab Said ambaye ni mkaazi wa kaunti hiyo akiongea na mwandishi wetu baada ya tangazo hilo alieleza jinsi hatua hiyo ya wagonjwa kuzuiliwa hospitalini inavyoathiri familia nyingi.

"Wakati mgonjwa amezuiliwa inabidi familia ianze kufanya mchango wa kutafuta pesa, unapata mtu wenu amepona lakini hivyo hivyo hakuna amani, kama agizo hilo litatekelezwa gavana atakuwa ametusaida sana," alisema Zainab.

Agizo hilo linatarajiwa kuanzia katika hospitali kuu ya Pwani ya Coast General kabla hospitali zingine kufuata mkondo huo, huku wakaazi wakipokea agizo hilo kwa furaha kubwa.