Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho ameipongeza idara ya usalama nchini kwa jitihada zake za kukabiliana mashambulizi ya kigaidi.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza baada ya shambulizi katika kituo cha polisi cha Central kutibuka siku ya Jumapili, Joho alisema ni bayana kwamba serikali kupitia idara ya usalama imejitolea kukabiliana na ugaidi, kwani maafisa wa usalama waliweza kuwaua washukiwa watatu kwa kuwapiga risasi.

Joho hata hivyo amesema tukio hilo ni aibu kwa serikali ya kaunti yake na serikali ya kitaifa, haswa ikizingatiwa kuwa waislamu kote duniani walikuwa kwenye pilkapilka za kujitayarisha kusherehekea sikukuu ya Eid-ul-Adha.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Evans Achoki alisema kuwa huenda makundi ya kigaidi yakawa yamebuni mbinu mpya za mashambulizi, huku akiwataka wananchi kutahadhari na kuwa makini zaidi.

Achoki pia alidokeza kuwa jaribio hilo la shambulizi lilitokea huku kukiwa hakuna taarifa zozoto za kijasusi zilizotoa tahadhari la shambulizi hilo.

Kufikia sasa, maafisa wa usalama wanaendelea kushika doria ili kuhakikisha wanakabiliana na aina yoyote ya utovu wa usalama.

Kufikia sasa, watu wanne wamekamatwa kuhusiana na shambulizi hilo.