Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewashukuru wawakilishi wadi kwa kupitisha mswada wa serikali ya kaunti kuwalipia ada maskwota wa shamba la Waitiki.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetenga takriban shilingi bilioni 1.2 ili kufanikisha mpango huo.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Alhamisi, Joho alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha maskwota hao wanapata nafuu kutokana na ada ya juu waliyoagizwa kulipa na serikali ya taifa.

Gavana Joho alisema kuwa waliamua kuchukua hatua hiyo kwa kuwa wakaazi wengi katika eneo hilo ni maskini na kipato chao ni cha chini ikilinganishwa na ada wanayotozwa.

“Hawa watu ni maskini sana. Kulingana na kipato chao, ni vigumu kulipia ada hiyo ambayo serikali kuu inawataka kuwatoza,” alisema Joho.

Aidha, Gavana Joho alisema kuwa ameunda kamati maalum itakayoongozwa na mkuu wa Idara ya Ardhi katika Kaunti ya Mombasa Anthony Njaramba, ili kufuatilia swala hilo.

“Kamati hii niliyounda itakuwa na jukumu la kudhibiti fedha hizo na kushughulikia taratibu zote wakati wa zoezi la kulipa ada hiyo,” alisema Joho.

Hatua hii ya serikali ya kaunti inakuja miezi kadhaa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru shamba hilo la Waitiki na kutoa hati miliki kwa maskwota hao.

Ni wakati wa hafla hiyo ambapo Rais Kenyatta alipotoa agizo kwa maskwota hao kuwa ni lazima walipe ada ya shamba hilo, kauli iliyopingwa vikali na viongozi kutoka serikali ya Kaunti ya Mombasa.