Gavana wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amewarai wakaazi wa Ukanda wa Pwani kuipinga serikali ya Jubilee katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Joho alisema kwamba serikali hiyo imeutenga Ukanda wa Pwani na wakaazi wa eneo la Pwani wanapaswa kuipinga serikali hiyo, huku akisema kwamba tayari upinzani umeweka mbinu za kuhakikisha kwamba unaingia uongozini.
"Nawaomba wakaazi wa Pwani msikubali kudanganywa na viongozi wa Jubilee na kuiunga mkono kwa sababu serikali hiyo haijawatambua wakaazi wa Pwani," alisema Joho katika mkutano wa kisiasa mjini Mombasa siku ya Jumatatu.
Kauli ya Joho iliungwa mkono na mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Mombasa Mishi Mboko aliyeikosoa serikali ya Jubilee kwa kumkandamiza gavana Joho.
Kwa upande wake, mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir aliwakashfu wanasiasa waliyouasi upinzani na kujiunga na mrengo wa Jubilee, huku akisema kwamba hatua hiyo inarudisha nyuma juhudi za viongozi wa Pwani katika kupigania haki za wakaazi wa eneo la Pwani
"Tunasikitishwa na viongozi tuliokuwa tumeamini kuwa wafuasi wetu lakini kwa kuwa wanatamaa ya pesa wamejitenga na sisi na kujiunga na Jubilee, viongozi kama hao sisi hatuwatambui na kamwe msikubali kunganywa na wao," aliongeza Abdulswamad.
Watatu hao walikuwa wakizungumza katika eneo la Mtongwe katika eneo bunge la Likoni baada ya kuzindua mradi wa barabara na ujenzi wa hospitali katika eneo hilo.