Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amewataka wakaazi wa Kaunti ya Mombasa na kaunti za Pwani kwa jumla kutoingiza siasa katika mipango ambayo serikali za kaunti zinajitahidi kuendeleza kote nchini.
Akizungumza siku ya jumamosi katika hafla ya uzinduzi wa ruwaza ya mwaka 2035 ya Kaunti ya Mombasa, katika ukumbi wa michezo wa Mombasa Golf club, Gavana Joho alisisitiza kwamba mipango ya maendeleo ya kaunti hiyo inanuia kuleta mabadiliko mengi katika Kaunti ya Mombasa ikiwemo kutoa nafasi za ajira kwa vijana, na hata kuinua kiwango cha mapato cha kaunti miongoni mwa faida nyingine nyingi zitakazotokana na mpango huo.
Kulingana na Gavana huyo, japo Kaunti ya Mombasa inakumbwa na changamoto nyingi, bado wakaazi wa Mombasa wana fursa nzuri ya kujiendeleza na kuendeleza kaunti.
Joho aliwataka wakaazi kuhusika katika miradi hiyo ili kuhakikisha kuwa miradi walionuia kutekeleza itakamilika.
Kauli hiyo liliungwa mkono na mwenyekiti wa tume ya kitaifa kuhusu ardhi Mohamed Swazuri ,ambaye alisema kuwa kuungana kwa serikali ya Mombasa ya ile ya kitaifa kutaipa nguvu zaidi kaunti hiyo ili iweze kuafikia malengo yake.
Swazuri pia aliwataka viongozi pamoja na wakaazi wa Kaunti ya Mombasa kuwa wenye busara na kutoingiza siasa katika miradi ya maendeleo.
Swazuri aliongeza kuwa wananchi kwa sasa wanakubwa na kasumba ya kutilia shaka kila mradi wa maendeleo ambao serikali za kaunti ama ya kitaifa inaanzisha katika kaunti mbalimbali.