Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho amewataka wanafunzi kuzingatia umuhimu wa elimu ili kuinua viwango vya elimu katika kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kwa ujumla.
Akizungumza siku ya Jumamosi katika hafla ya kuwatuza wanafunzi bora waliofanya mtihani wa kitaifa wa shule za msingi na upili kutoka eneo la kaunti ndogo ya Mvita katika shule ya upili ya Burhania ambapo alikuwa mgeni mheshimiwa, Joho aliwapongeza wanafunzi wote walioshiriki mitihani ya kitaifa huku akisema kwamba kaunti yake ina nafasi kubwa ya kufanya vyema kama kaunti nyengine nchini kwani kufikia sasa idadi ya wanaojiunga na shule za upili inazidi kuongezeka ikilinganishwa na hapo awali.
Aidha Joho aliwataka wanafunzi ambao hawakuweza kufikisha kiwango cha kupata nafasi katika vyuo vikuu kujiunga na taasisi mbambali nchini na hata pia kujiunga na kosi ndogondogo kulingana na matokeo yao huku akisema kuwa kutofikisha alama za kujiunga na vyuo vikuu si mwisho wa ndoto ya mtu mwenye.
Hata hivyo kwenye sherehe hizo, tuzo zilitolewa kulingana na wanafunzi bora katika somo, mwalimu bora kulingana na matokeo ya mtihani wa kitaifa na shule bora kama ilivyotolewa na kamati inayosimamia maswala ya elimu katika kaunti ndogo ya Mvita.
Picha: Gavana wa Mombasa Hassan Joho akimkabidhi tuzo mwalimu katika kaunti ndogo ya Mvita siku ya Jumamosi. Amewataka wanafunzi kuzingatia umuhimu wa elimu ili kuinua viwango vya elimu katika kaunti ya Mombasa na eneo la Pwani kwa ujumla.