Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Mombasa Ali Joho ametoa wito kwa mashirika kuwapa nafasi vijana kuonyesha uchuzi wao katika sekta mbalimbali, na akaitaka serikali ya kutaifa kuwekeza zaidi kwenye sekta ya uhandisi kama njia mojawao ya kuunda nafasi za kazi miongoni mwa vijana.

Amesema kwa kuwa na viwanda vya kutengeza bidhaa na kuwapa vijana kazi za utaalam vijana wenye ujuzi mbali mbali ambao wamemaliza vyuo, itakuwa hatua kubwa kueleke kufanikisha maono ya milenia na azimio la mwaka wa 2030.

Akiongea siku ya Jumatano wakati wa uzinduzi wa feri mpya iliyondwa na kampuni moja yenye makao yake huko Likoni katika kaunti ya Mombasa, Joho alisema kuwa wakati umefika vijana kutoka nchini kupewa imani na nafasi mwafaka ya kuunda bidhaa kama hivyo walionyesha ya kutengeneza feri hiyo ambayo inaelekea kufanya kazi katika nchi jirani ya Uganda.

Gavana Joho alizitaka kampuni zilizoko katika miji yote nchini kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha ujuzi wao ili katika siku zijazo, isiwe na utegemezi wa mara kwa mara kwenye wataalam wa nchi za magharibi.

Gavana huyo alisema kuwa atafanya kila awezalo kuona kuwa vijana wanapewa nafasi, na kuishuru kampuni ya Secco kwa kuwaamini wakenya kwa kuwapa nafasi ya kuunda mitambo kama hiyo, ambapo vile vile alidokeza kuwa serikali yake iko tayari kushirikiana na washika dau ili kuinua uchumi wa kaunti hiyo.